Kwa mujibu wa ripoti ya Kitengo cha tarjuma cha Shirika la Habari la Hawza, Ben-Dror Yemini, mchambuzi wa Kizayuni, katika makala yake iliyochapishwa na gazeti la Yedioth Ahronoth, amezungumzia “kushindwa kimkakati kwa Marekani” kupitia makubaliano yaliyofikiwa na Iran kwa ajili ya kusitisha vita, na kusisitiza kwamba; makubaliano hayo “hayafanyi chochote isipokuwa kuimarisha nafasi ya Iran na Hizbullah.”
Mchambuzi huyo wa Kizayuni, katika makala yake kuhusu “kushindwa kimkakati kwa Marekani” kutokana na makubaliano yaliyofikiwa na Iran ya kusitisha vita, amesema kuwa; makubaliano hayo yanazungumzia Iran na Lebanon kwa pamoja kama sehemu ya mwisho wa vita, lakini mwisho huo hauna matokeo mengine isipokuwa kuimarisha nafasi ya Hizbullah, kama vile unavyoimarisha nafasi ya Iran.
Akiashiria kwamba kadiri maelezo ya mwisho na rasmi ya makubaliano hayo yanavyozidi kuwekwa wazi, ndivyo wasiwasi unavyozidi kuongezeka, Yemini alisisitiza kuwa; mambo haya si uvumi tena; bali makubaliano hayo katika baadhi ya vipengele ni mabaya zaidi hata kuliko vifungu 14 ambavyo vilikuwa vimevuja hapo awali.
Katika muktadha huo, Yemini alibainisha kuwa pengo kati ya kauli za Rais wa Marekani Donald Trump na uhalisia wa mambo “halijawahi kuonekana kubwa kiasi hiki.” Alisema kuwa; pengo hilo linatia wasiwasi mkubwa na linaibua hofu kwamba huenda kuna tatizo katika tathmini za Trump pamoja na watu wake wawili wa karibu na waaminifu zaidi, yaani Steve Witkoff na Jared Kushner.
Alisisitiza kuwa; vipengele vya makubaliano hayo vinaonesha wazi kwamba “Iran ndiyo mshindi mkubwa zaidi.”
Wakati ambapo Trump hapo awali alikuwa ametangaza kuwa moja ya malengo ya vita ni kuharibu akiba ya makombora ya balestiki ya Iran pamoja na uwezo wake wa kuzalisha makombora hayo, jana alibadili msimamo wake kabisa na kusema kuwa hakuna tatizo ikiwa Iran itaendelea kuendeleza makombora ya balestiki, kwa sababu nchi nyingine pia zinamiliki makombora ya aina hiyo.
Yemini alihoji kuhusu kauli hiyo akisema: “Makumi ya mamilioni ya watu wanamsikiliza na hawaamini wanachosikia… Je, huyu ndiye kweli rais wa dola yenye nguvu zaidi duniani? Je, amepoteza akili zake?”
Kauli hizi zimekuja kufuatia kufikiwa kwa matini ya mwisho ya makubaliano ya kusitisha vita katika eneo kati ya Iran na Marekani; makubaliano ambayo yameanza kutekelezwa kupitia saini za kidijitali za pande zote mbili. Hata hivyo, kwa mujibu wa tathmini za Wazayuni, makubaliano hayo “yanajumuisha janga na kushindwa kwa kimkakati kwa Israel.”
Kwa mujibu wa makala hiyo, makubaliano hayo yanajumuisha vifungu 14, ambapo muhimu zaidi ni: Kusitishwa kwa operesheni zote za kijeshi katika medani zote za muqawama, ikiwemo Lebanon.
Kuanza kwa mchakato wa mazungumzo kwa ajili ya kufikia makubaliano ya mwisho ndani ya siku 60 zijazo.
Maoni yako